Thursday 21 July 2011

UTAMADUNI WA KUTOWAJIBIKA, KULEANA, KUOGOPANA NA KUONEANA HAYA

Waafrika tuna tamaduni nyingi ambazo japo hatupendi watu watuambie ama watukumbushie kuwa tunazo zimesababisha udumavu wa maendeleo katika taswira nzima ya maisha jamii yetu. Utamaduni wa kutowajibika katika majukumu tunayojipa sisi wenyewe ama tunayopewa na watu wengine. Hatuna uchangamfu katika kazi yeyote ile tunaona kufanya kazi ni kupoteza muda ambao tungeutumia vizuri kupumzika huku tukinywa vinywaji tunavyopenda na tukiwa katika mazingira ya starehe.

Kuanzia muuza chipsi na mtengeneza kandambili uswahilini mpaka mawaziri katika mawizara hali ndio hiyo hata kama mtabisha maana hili la ubishi sisi ni nambari moja. Tutabisha hata kama jambo liko wazi kama jua la mchana wa saa sita. Tunafanya kazi bila ya umakinifu yakinifu bila ya shauku ya kuboresha tulilofanya jana tutalirejea leo kama ilivyokuwa jana. Tunafanya kazi kama mashine (robot) hatutumii fikra zetu kuboresha huduma ila tuna ubunifu mkuu wa kupindisha miongozo ili tupate njia ya kutoza rushwa kwa huduma tunazotoa.

Uswahilini mpaka maofisini na viwandani na hasa serikalini tuna utamaduni wa kuleana na kuogopana. Wengi wenu mnaona makosa yanayofanyika katika sehemu zenu za kazi lakini ulezi umewazidi na mnaona kwamba mkisema juu ya kosa hilo basi mtakosana na mkosaji na kwasababu hakuna mazingira ya kuadabishwa basi bora tu mgawane makosa. Hii huzaa woga kwamba wewe una siri ya Yule na Yule ana siri yako kwa hiyo wote mnakaa kimya na kulindana kwasababu ya woga wa kuvuja kwa siri mlizowekeana.

Hii huleta kushuka kwa ufanisi kazini na pia uvunjaji mkubwa wa sheria za kazi na watu kujifanya miungu watu. Unakwenda kupata huduma ambayo unalipia lakini unajikuta kama vile ile huduma umepewa bure kutokana na dharau na usumbufu utakaopata. Ukienda mahospitalini makarani hujifanya ndio madokta kwa maana bila ya kuwapa kitu kidogo huwezi kumuona dokta. Mara utaambiwa faili lako limepotea wakati ulilifungua dakika kumi zilizopita. Una ugonjwa wa kufa utaambiwa daktari hayupo lakini ukitoa kidogo kama miujiza daktari anatokea.

Hata ukienda madukani kununua bidhaa wauzaji wanakupa dharau kama vile hizo bidhaa unanunua kwa bei ya bure na wao wanakufanyia hisani kukuuzia.
Ukienda wizara ya mambo ya ndani huko ndio usitoe pua kabisa kuomba passport imekuwa ni mradi unaojenga mahekalu mbezi na kwengineko. Utaambiwa wewe si mtanzania hapo ndipo utakapo koma, unaweza kuhisi wewe ni mkimbizi kwenye nchi yako wakati wachina wanakupita na mikoba ya baba Kambarage.
Alama za vidole huchukuliwa wahalifu ili wapate kutambulika kirahisi wanaporudia makosa.Kuomba pasi ya kusafiria imekuwa kosa ama wewe ni mhalifu mtarajiwa na utajiuliza sasa haya madole mnayochukua ni ya faida gani wakati mijambazi kibao na mijizi iliyojaa mtaani hamujawahi kuikamata kwa kutumia alama za midole hii wajameni...hii ni kutokana na utamaduni wetu wa kuogopana tunaogopa kuwaambia wamarekani na ndugu zake kuwa hatuwezi kuuza alama za wananchi wetu kwa bei ya dola moja.

Tunaoneana haya kiasi watu wamekuwa wakitovuka adabu kupita mifano kwasababu wanajua na wewe unajua kuwa huwezi kumfanya kitu.hii ni kama maigizo ya Simba kumuogopa Swala..ni hivi hivi nchi inazama tunaoneana haya kuambizana kwamba ili mashua yetu iende mbele inabidi tupige makasia. Wakubwa wanakula marushwa halafu wanawekeana viporo mara kimya kama ubaridi wa asubuhi unapopiga usoni na ukaendelea kuvuta shuka.

Kwa utamaduni huu maendeleo hayaji n’go kama mvua jangwa la sahara tutaendelea kuungua na jua mpaka dunia ibadili egemeo. Yangu ni macho ila utamaduni huu utatupeleka pabaya maana wanaofaidi ni wachache na wengi tunaumia. Wengi tunaingia makanisani na misikitini ili tuonekane tuna dini lakini ukweli ni kwamba hatuna imani wala dini..Dini yetu ni Ubinafsi na Mungu wetu ni Fedha..Tushauza roho zetu kwa shetani ili tupate Fedha, tunaua wenzetu ili tupate Fedha, tunadhulumu wenzetu ili tupate Fedha.. hatujali mwengine zaidi yetu na yote haya kwasababu ya KULEANA na KUOGOPANA..

No comments: