Wednesday 12 January 2011

Kilimo kwanza na sera za vichwa maji


Jana nilibahatika kumsikiliza Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania alipotembelea London. Katika Mazungumzo yake moja ya ujio wake ilikuwa kumuaga aliyekuwa balozi hapa London Bi Maajar. Pia aligusia mipango ya serikali katika jitihada za kuleta maendeleo ya nchi kupitia KILIMO.

Nilifurahi kuona Mheshimiwa anaelewa vyema kuwa JEMBE la mkono halitotufikisha mbali. Suala ni njia gani zitumike ili mabadiliko ya kweli ya kilimo yatokee... Hili ni suala zito kwa maana inahitaji mipango madhubuti itakayoshirikisha wadau na wana sayansi wa kilimo na sayansi nyenginezo ili kuleta jawabu litakalofaa kusukuma gurudumu hili zito. Tatizo lililopo Waafrika kwa ujumla tumekosa MWAMKO (PASSION) ya kufanya jambo likafanikiwa.

Tumebweteka na kutaka matokeo ya kazi yaonekane hapo hapo kwa ujumla tumekosa subira. Na hili limetufanya tuogope kufanya miradi ya muda mrefu. Tumeweka ujira mbele kuliko ajira yenyewe. Tunataka malipo kabla hata biashara haijauzwa. Na kwa mtazamo huu hatufiki popote.

Serikali hata ikawa na mipango thabiti ya kutokomeza umasikini kama hakuna watekelezaji wa mipango hiyo itakuwa ni kama hadithi isiyokwisha. Passion ndio ilofanya watu wakagundua Umeme. Passion ndio ilofanya watu wakagundua Machine. Passion ndio siri ya maendeleo ya nchi za magharibi.

Kuna watu wanatumia maisha yao yote kuchunguza kitu kimoja mpaka waone mwisho wake. Na mara nyingi jitihada hizo hulipa na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii wanazoishi. Na malipo yao ni zaidi ya pesa, Hutajwa na hawatosahaulika mpaka mwisho wa dunia kutokana na michango yao. JEE SISI TUNAWEZA HAYO...? Jibu tunaweza ila inabidi tubadilike ila je wangapi wanapenda mabadiliko? Jibu ni wachache tushazoea maisha ya kuzugazuga. WASEMAJI GUNIA WATEKELEZAJI PUNJE...

No comments: